Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba huduma za dawa za ARV za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI zinapatikana bure kwa wagonjwa wote.
Kauli hiyo ameitoa leo, Februari 20, 2025, wakati akishiriki katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo uliofanyika mkoani Lindi. Uzinduzi huu umezinduliwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Deriananga, kwa niaba ya waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na viongozi wengine na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya afya ambapo amesema Serikali imetumia zaidi ya bilioni 48 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, ikiwa ni pamoja na hospitali, vituo vya afya na zahanati katika mkoa wa Lindi na maeneo mengine nchini.
Aidha, Dkt. Mollel kwa sasa huduma za kibingwa, ikiwemo matibabu ya uvimbe wa ubongo bila kupasua kichwa na matibabu ya kansa ya ubongo kwa kutumia sauti maalum, zinapatikana nchini Tanzania ambapo upatikanaji wa huduma hizi za kibingwa hapo awali zilikuwa zikipatikana kwa shida au kutoonekana kabisa.
Mradi wa Timiza Malengo awamu ya tatu unalenga kuboresha sekta ya afya na unasimamiwa katika halmashauri 36 za mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambapo mikoa ya Dodoma, Geita, Lindi, Mara, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Singida, Tabora, na Tanga inahusika. 
Mradi huu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuboresha mazingira ya huduma za afya kwa wananchi wote, huku Serikali ikijitahidi kutekeleza malengo ya kuleta maendeleo kwa wananchi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini.
Mwisho, Dkt. Mollel amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huduma za afya zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi, huku akiwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao ili kuepuka magonjwa yanayoweza kuzuilika.



 
 
 
 
0 Comments