Marekani na Israel zasema kundi la Hamas lazima liangamizwe


 Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio wamekutana mjini Jerusalem huku Wapalestina wakilikimbia eneo la kaskazini kutokana na mashambulizi makali ya Israel.               Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na kufanya mazungumzo hii jana Jumatatu mjini Jerusalem na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio. Viongozi hao wametoa kauli inayosisitiza juu ya kuliangamiza kundi la Hamas na kuachiliwa mateka wote wanaoshikiliwa kwa ajili ya amani huko Gaza.

Rubio pia ameiambia Israel kwamba Marekani inaunga mkono "jukumu lenye tija" la Qatar katika upatanishi huko Gaza, baada ya Israel kulishambulia taifa hilo la Ghuba.

Netanyahu ametetea shambulio hilo akisema liliwalenga viongozi wa Hamas.

Ziara ya Rubio ya siku mbili inalenga kuonyesha uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ambayo inakabiliwa na kutengwa kabla ya nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Mataifa kulitambua taifa la Palestina. Netanyahu anapinga vikali utambuzi huu.

Rubio aliwasili Israel hapo jana Jumapili huku nchi hiyo ikizidisha mashambulizi kaskazini mwa Gaza.

Wakaazi wa eneo hilo wanahangaika kuhama kutokana na amri ya jeshi Israel inayowataka kuuhama mji huo. Wengi wao wameliambia shirika la Habari la AFP kwamba hawana mahala pengine pa kwenda.

Wakati huo huo viongozi wa nchi za Kiarabu wanakutana hii leo mjini Doha, Qatar kwa ajili ya mkutano wa dharura ikiwa ni wiki moja baada ya mashambulizi ya Israel yaliyowalenga viongozi wa kundi la Hamas nchini Qatar. Mashambulizi hayo yamesababisha hasira kubwa.

Mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ulioitishwa na Qatar unalenga kuiwekea shinikizo Israel, ambayo imekuwa inakabiliwa na miito inayoongezeka ya kuvimaliza vita na mgogoro wa kibinadamu huko Gaza.

Kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bib Hamad al-Thani, ameuambia mkutano huo kuwa inachotaka Israel ni kuyafanya mataifa yote ya Kiarabu kuwa chini ya udhibiti wake na kwamba haina nia yoyote ya kupatikana amani baina yao na Wapalestina. Kiongozi huyo ameongeza na hapa namnukuu: "Mtu yeyote anayedhamiria kwa makusudi kabisa kuwauwa wale anaojaribu kufikia nao makubaliano, anakusudia kuyachafua majadiliano hayo. Kwake yeye, mazungumzo ni sehemu tu ya vita." Mwisho wa kumnukuu.

Kwa upande wa Hamas, afisa wake mkuu Tahir al-Nono amesema mazungumzo ya kubadilishana wafungwa yamesitishwa na kwamba hayawezi kuendelea kutokana na wajumbe wake wanaohusika na mazungumzo hayo kushambuliwa ndani ya nchi ambayo ni mpatanishi.

Post a Comment

0 Comments