Jaji mmoja nchini Marekani ameuzuia utawala wa Trump kuchukua hatua zozote za kulifunga Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Katika uamuzi wake Jumanne, Jaji Theodore Chuang alisema juhudi zinazoongozwa na Idara ya Ufanisi ya Serikali ya mshirika wa Trump Elon Musk (Doge) kulifunga shirika hilo huenda zilikiuka katiba ya Marekani "kwa njia nyingi".
Jaji huyo pia aliamuru kwamba kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wa USAID kunapaswa kukomeshwa, lakini hakuamuru kurejeshwa kazini kwa wafanyikazi waliowekwa likizo hapo awali.
Uamuzi huo unajiri katika kesi iliyowasilishwa kwa niaba ya wafanyakazi 26 wa USAID ambao hawakutajwa majina wanaodai mahakamani kwamba Musk anafuata "mtazamo wa kutabirika na usiojali wa kufyeka na kuchoma"
katika kuvunja idara za serikali ya Marekani.
Katika malalamiko yaliyowasilishwa tarehe 13 Februari, mawakili wa wafanyikazi hao walidai kuwa mamlaka ya Musk sio halali - kwani hajateuliwa rasmi katika wadhifa wa serikali wala kuthibitishwa na Seneti ya Marekani - na kuomba shughuli za Doge zisimamishwe na kubadilishwa.
USAID ilikuwa mojawapo ya mashirika ya kwanza kulengwa na Doge muda mfupi baada ya Trump kuingia tena White House mwezi Januari na kuamuru kusimamishwa kwa siku 90 kwa misaada yote ya kigeni ya Marekani.
Musk na Doge walibishana kwenye hati za korti kwamba jukumu la Musk lilikuwa ni la ushauri tu.
Lakini Jaji Chuang aliamua kwamba Musk na Doge walidhibiti USAID na kwa kufanya hivyo "huenda walikiuka Katiba ya Marekani kwa njia nyingi, na kwamba hatua hizi zilidhuru sio tu walalamikaji, bali pia maslahi ya umma." Haijulikani ni matokeo gani uamuzi huo utakuwa na athari kwa shughuli za USAID.

 
 
 
 
0 Comments